Somo la Kwanza: Isa 50:4-7
Somo la Pili: Phil 2:6-11
Injili: Mat 26:14–27:66
Somo la Kwanza: Isa 50:4-7
Somo la Pili: Phil 2:6-11
Injili: Mat 26:14–27:66
Utangulizi
Leo Jumapili ya Matawi au Jumapili ya mateso ya Bwana. Kipindi chetu cha kwaresma tulichokianza Jumatano ya majivu kinapata nguvu zaidi katika maadhimisho ya liturujia ya Juma Kuu, ambapo kilele chake ni Pasaka. Ibada za Juma kuu zinazoambatana na ishara za nje za pekee kama matawi – zituzamishe zaidi katika fumbo la wokovu, uhusiano wangu na Mungu.
Homilia
Dominika ya Matawi inaonyesha shangwe juu ya Yesu akiwa anaingia Yerusalemu. Liturujia ya siku ya leo imeundwa na sehemu mbili tofauti zenye kuleta hisia tofauti. Kuna Liturujia ya utukufu na shangwe kuenji jinsi Yesu alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe na kuimbiwa “hosanna hosanna juu Mbinguni.” Watu walifurahi kwa shangwe Yesu alipoingia Yerusalemu. Sehemu ya pili, taratibu hali ya shangwe inabadilika tunapoingia kwa undani katika masomo yetu.
Somo la I: Katika somo la kwanza tunapewa maono ya mtumishi wa Bwana anayeteseka. Mtumishi huyu anateseka si kwa makosa yake, bali bila kosa na zaidi anateseka kwa ajili ya wengine. Anateseka pia kwa hiari yake.
Somo hili linatupa picha na kutuonyesha hali ile ile aliyokuwa nayo Yesu, mtumishi wa Mungu, aliyeteseka ili atusaidie sisi sote. Hakurudisha kisasi, hakulalamika, wala kulaumu au kujionea huruma. Mateso na uchungu vimekuwa nyenzo ya kuonyesha upendo kwa Baba na kwetu. Ukaribu wa kweli na Mungu unahitaji uvumilivu uvumilivu na utii hata katika mateso.
Somo la II: Paulo anatuonyesha fadhila ya unyenyekevu ulivyoletwa na Kristo. Kristo alikuwa na hali ya Mungu, lakini hakung’ang’ania, alijinyenyekeza akawa mtii, hata mauti ya msalaba.
Unyenyekevu na kujitoa ndio njia ya kuwa karibu zaidi na Mungu. Kristo hakung’ang’ania kuwa sawa na Mungu, bali alikuja karibu nasi. Akakubali mateso hata kufa msalabani. Na Mungu akamwinua juu kabisa, akampa jina lililo kuu kabisa. Kipindi hiki tumekuwa tukijifunza unyenyekevu na basi tuuishi.
Injili: Injili inasimulia mateso ya Yesu, kusalitiwa, kukamatwa, kuhukumiwa, kudhihakiwa, kusulubiwa na kufa msalabani kwa ajili ya wokovu wa wanadamu.
Upendo wa Kristo unaonekana katika kujitoa msalabani. Yesu hakulazimishwa kwenda msalabani. Alijitoa kwa hiari yake kwa ajili ya wokovu wetu. Alisasalitiwa, akakataliwa, na akahukumiwa bila haki. Alikubali kutimiza mapenzi ya Baba yake. Ndipo anapotufundisha na sisi kujitoa kwa ajili ya wenzetu bila kudai maslahi. Hata inapobidi sadaka kubwa. Ndipo tutakapokubali kubeba misalaba yetu pia.
Udhaifu ama dhambi ya mwanadamu inaonekaka katika mateso ya Kristo. Katika masimulizi ya mateso ya Kristo tunaona dhambi nyingi ya mwanadamu. Pilato anamuhukumu ingawa haoni kosa lake. Petro anamsaliti, Yuda anamsaliti, Viongozi wa dini wanamuhukumu kwa wivu na chuki, Yuda anamuuza na kumsaliti. Sisi pia tunajikuta katika dhambi hizo katika jamii. Kusalitiana, kudhulumiana, kuwahukumu wengine, kushindwa kupokea ukweli n.k
Msalaba ni njia ya wokovu na mafanikio. Kifo cha Yesu msalabani si mwisho bali mwanzo wa wokovu. Ilionekana laana, bali sasa imekuwa ushindi. Msalaba umefunua utukufu wa Mungu. Kutoka katika mateso kulizaliwa wokovu. Katika maisha yetu pia tuukumbatie msalaba. Tusiogope kupitia mateso. Tuyaunganishe na msalaba wa Yesu nasi tutashinda. Tumwombe Mungu atujalie kwa fumbo la msalaba kukaa karibu naye zaidi na kujipatanisha naye.