Somo la Kwanza: Eze 37:12-14
Somo la Pili: Rom 8:8-11
Injili: Yn 11:1-45
Somo la Kwanza: Eze 37:12-14
Somo la Pili: Rom 8:8-11
Injili: Yn 11:1-45
Utangulizi:
Mungu ndiye chanzo cha uzima. Mungu wetu kupitia Bwana wetu Yesu Kristo ana mamlaka juu ya wazima na wafu. Anao uwezo wa kuhuisha tena kilichokufa. Mungu anairudishia mifupa mikavu uhai, Yesu anamrudishia Lazaro uzima tena. Tunaalikwa kumtumania Mungu anao uwezo wa kutuhuisha tena toka katika mauti.
Homilia:
Katika safari yetu ya Kwaresma tunaletewa ujumbe wa uzima dhidi ya mauti. Dhidi ya mambo yaliyoshindikana. Mungu anakwenda kufungua vifungo vya dhambi, vya mauti, vya hali yetu ya kufa kwa kifo cha Mwanae Bwana Wetu Yesu Kristo.
Somo la I: Katika somo la kwanza tunasikia maono ya nabii Ezekiel ya mifupa mikavu. Mungu anaahidi kufungua makaburi yao na kuwarudishia tena uzima kwa kuweka roho wake ndani yao.
​Katika somo la kwanza tunakumbushwa na maneno ya malaika Gabriel aliyomwambia Bikira Maria kuwa “Kwa Mungu hakuna lisilowezekana.” Mungu anaonyesha uwezo wa wake wa kuuisha na kufanya tena upya kile kinachoonekana kimekwisha kabisa ama hakuna matumaini tena. Hii ilikuwa picha ya taifa la Israel lililokuwa limevunjika moyo uhamishoni, limekata tamaa kabisa mithili ya mifupa iliyokauka hakuna matumaini tena ya uhai.
​Katika maisha yetu pia ipo imani iliyokufa, matumaini yaliyopotea, mazingira magumu, mahusiano yaliyovunjika. Kumbe kipindi hiki ni wakati wa kumruhusu Mungu afufue maisha yetu, atupe matumaini mapya tena, aturudishie furaha tena, aturudishie uhai tena tuliopoteza kwa dhambi zetu.
Somo la II: Katika somo la pili Mtume Paulo anatufundisha kuwa Roho Mtakatifu ndiye anayetupa uzima mpya ndani yetu. Anatuonyesha tofauti ya kati ya kuishi kwa mwili na kuishi kwa mwili. Kuishi kwa mwili kunamaanisha kufuata tamaa za mwili na ubinafsi. Kuishi kwa roho ni kuishi katika uhusiano na Mungu.
​Roho Mtakatifu anayekaa ndani yetu ndiye anatupa nguvu ya kuishi maisha mapya. Hata kama miili yetu inakufa, Roho wa Kristu anatupa uzima. Tunaalikwa kuchagua Maisha katika Roho badala ya maisha ya mwili. Maisha ya Roho ndiyo maisha ya neema, maisha ya kuzitakasa roho zetu.
Injili: Katika somo la Injili linatimiza maono ya nabii Ezekiel kuwa Yesu anao uwezo juu ya mauti, Juu ya maumivu, juu ya uchungu, juu ya majonzi. Yeye ndiye ufufuo na uzima. Yesu anadhihirisha hilo kwa kumfufua Lazaro. Alikuwa amekufa na kuzikwa siku nne. Hata kama alikuwa ameoza anapata uhai tena. Alikuwa anaanza kutoa harufu ananukia tena. Yesu anatuonyesha kuwa anashiriki hali yetu ya kibinadamu na kututoa katika mauti, vifungo, na mashaka na uhakika wa uzima wa milele.
​Yesu anatufundisha kuwa – Yeye ndiye ufufuo na uzima. Hii ndiyo kweli tunayotakiwa kusadiki si tu hadi ujio wa wake wa pili bali sasa. Tukikubali kumkiri Kristo anatutoa katika uvuli wa mauti.
​Yesu anatutaka tutoe jiwe lililotuzuia katika maisha yetu. Pengine lipo jiwe linalotuzuia tunafunikwa katika uvuli wa mauti. Tunashindwa kumwona Yesu, tunanuka, watu wanatuhuzunikia, Yesu anatuamuru tulitoe. Jiwe hilo ndilo kufa kiroho, pengine zindiko, tambiko, wizi, uchumba sugu, uzinzi, uasherati n.k. Tunapolitoa tunakuwa hai tena.
​Yesu anashiriki ubinadamu wetu katika hali zetu. Yesu hili analionyesha katika kushiriki huzuni ya Martha na Maria juu ya Lazaro. Yesu anataka umshirikishe hali yako, haijalishi ni ngumu kiasi gani. Yeye Ndiye ufufuo na uzima. Ukihisi hali ya mauti mwambie, ukihisi huzuni mwambie, kuumwa mwambie. Jenga urafiki naye kwa kumshirikisha hali zetu hadi alie kwa ajili yako.
​Tumwombe Mungu atujalie kukubali kuhuishwa naye. Kutoka katika hali ya umauti wa dhambi na kufanywa tena upya kwa toba ya kweli, sacramenti ya kitubio na katika kukutana na Yesu katika Ekaristi Takatifu.