Kiu ya Mungu Haiwezi kutulizwa Pasipo Mungu Mwenyewe

2026-03-08
Dominika ya 3 ya Kwaresma
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Kut 17:3-7

Somo la Pili: Rom 5:1-2, 5-8

Injili: Yn 4:5-42

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Roho zetu hazitatulia hadi zitakapotulia kwa Mungu. Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuliza hamu na kiu ya mwanadamu. Ndiye chemchemi ya Maji ya uzima. Tukimkaribia kwa imani na kumruhisu Kristo aingie katika maisha yetu, tunabadilika na kuwa mashahidi wa jirani.

Homilia

Katika Dominika hii ya tatu tunapata picha ya maji yanayotuliza kiu ya mwanadamu ambapo, Kristo ndiye anayetupa maji ya uzima yanayotuliza kiu halisi ya maisha yetu. Mwanadamu huwa na kiu sit u ya maji ya mwili bali pia ya roho.

Somo la I: Waisraeli walipokuwa jangwani walikosa maji wakaona kiu wakaanza kumnungunikia Musa. Mungu akamwambia Musa apige mwamba kwa fimbo yake, na maji yakatoka watu wakanywa.

       Mungu hutoa maji hata pale ambapo imani yetu ni ndogo ama imedhoofika kabisa. Wana wa Israeli waliingiwa na hofu, mashaka, wasiwasi, kukata tamaa, kulalamika na hata kumjaribu Mungu. Hili linaonyesha udhaifu wa mwanadamu. Mara nyingi tunamsahau Mungu tunapokutana na shida, changamoto au matatizo.

       Katika somo la kwanza tunajifunza mambo mawili muhimu: Kwanza unapopatwa na shida au changamoto leo, usisahau wema wa Mungu aliokutendea jana. Mungu mwenyewe ndiye anayetutimizia kiu yetu ya maisha. Wana wa Israel walisahau kuendelea kukazia macho kule Mungu alikotaka wafike, Huruma ya Mungu ikawasaidie ili waweze kutimiza alichotaka Mungu tangu mwanzo – Kufika nchi ya ahadi na kumwabudu Mungu wa kweli.

Somo la II: Paulo anatukumbusha kuwa tumepatanisha na Mungu kwa njia ya Kristo. Si kwa sababu tunastahili hapana ni kwasababu ya upendo wake Mungu na Neema zake juu yetu. Upendo huo ulionekana wazi pale Kristo alipotoa maisha yake kwa ajili yetu pale msalabani. Hivyo Mungu anatupenda vile tulivyo licha ya udhaifu wetu. Thibitisho hilo linaonekana kwa Kristo kufa msalabani.

       Njia yetu ya kuifikia nchi ya ahadi, kuifikia kiu yetu ya mioyo yetu na roho zetu ni Kristo. Upendo wake kwetu ndio chemchem ya uzima na tumaini la maisha yetu.

Injili: Katika somo la Injili tunasikia simulizi la Yesu na mwanamke Msamaria. Mama huyu anakutana na Yesu na anabadili maisha yake na mtazamo wa Wayahudi. Pengine haikuwa kawaida kwa mazingira ya kawaida kwenda kisimani majira ya mchana. Hata katika mazingira yetu isipokuwa ni asubuhi au join mchana sio muda mzur wa kina mama kuchota maji kisimani, kama si dharura. Lakini pengine wokovu wake ndio uliomsukuma kwenda kisimani kama tunavyoshuhudia katika hadithi hiyo. Mungu akiwa anapoona kiu ya imani yako hata katika mazingira yasiyo ya kawaida anakuokoa. Mambo machache ya muhimu katika Somo la Injili ni kwamba:

       Kristo ndiye anayetuliza kiu yetu ya maisha. Ndiye anayetupa maji ya uzima wa milele. Anatunywesha na kutulisha. Tunapokunywa na kula mwili wake katika Sakramenti Takatifu na katika neno lake hatupati kiu tena, tunapata uzima wa milele.

       Tunapokutana na Kristo kweli katika maisha yetu lazima kubadilika. Mama huyu anageuza mwenendo wake na kuwa mmisionary wa Injili kwa Wasamaria wenzake. Anaacha njia yake ya dhambi, kuwa na wanaume watano, na kuamua kupata wokovu katika maisha yake.

       Kristo anavunja matabaka katika maisha yetu. Yesu anatuonyesha kuwa, hata Wasamaria walioonekana hawafai, wanastahili wokovu. Kristo anavunja tabaka hilo kwa kumwokoa na dhambi na mtazamo wake. Kristo anachoangalia ni kwamba tumeacha dhambi na kubadilika na sio sisi ni wa wapi ama ni kina nani katika jamii.

       Mfungo wetu wa Kwaresma ni kipindi cha ni kipindi cha kutukumbusha kuwa kiu yetu iwe ni kwa kuutafuta uzima wa milele. Kumwabudu Mungu katika Roho na Kweli. Kutamani kukutana na Yesu atupe maji ya uzima wa milele. Na hivyo kubadili mienendo yetu isiyofaa na kuwa wamisionari wa Injili ya Bwana.