Somo la Kwanza: Mwa12:1-4
Somo la Pili: 2 Tim 1:8-10
Injili: Mat 17:1-9
Somo la Kwanza: Mwa12:1-4
Somo la Pili: 2 Tim 1:8-10
Injili: Mat 17:1-9
Utangulizi
Mungu anatutuma kutoka katika maisha tuliyoyazoea na kuingia katika nchi anayotaka yeye. Anatutaka tutoke katika jangwa alipo shetani hadi mlimani alipogeuka sura Yesu. Toba ya kweli, sadaka, mfungo, sala na matendo ya huruma vituwezeshe kupiga hatua kiroho na kimwili.
Homilia
Safari yetu ya toba ya kweli, kusali, kufunga na matendo ya huruma iwe zaidi ni safari ya kutuingiza katika utakatifu. Kuingia kwenye utukufu wa Mungu. Kipindi hiki kinatupa fursa ya kuondokana na mazoea ya zamani na kupanda mlimani pamoja na Kristo.
Somo la I: Katika somo la kwanza Mungu anamwita Abramu aondoke katika nchi yake aliyoizoea, na jamaa zake, na nyumba yake na baba yake aende katika nchi atakayomwonyesha. Ni wito mgumu lakini uliojaa matumaini na imani. Licha ya uzee na mazingira aliyozoea Abramu ambiwa atoke.
Ni wito wa kuanza upya, kuisikiliza sauti ya Mungu, kujitoa sadaka, kuacha yote kwa ajili ya Mungu. Mungu anamuhakikishia Abramu; i) kuwa atakuwa taifa Kubwa, ii) atakuwa baraka kwake na kwa jamaa zake na dunia nzima, iii) Ulinzi wa Mungu- atakayembariki – Mungu atambariki, - atakayemlaani – Mungu atamlaani.
Tukiachana na uzamani na dhambi – Mungu anatuhakikishia taifa kubwa, baraka, baraka na kwa familia zetu, na ulinzi wa Kimungu.
Somo la II: Paulo katika somo la pili anamsihi Timotheo kuwa wito Mtakatifu ni kuihubiri Injili. Na katika kuitikia wito wa Mungu tujikabidhi chini yake atuongoze kwa nguvu yake. Katika Kristo ndipo tunatakiwa kujikabidhi kwake ili tuweze kutenda kadiri ya mapenzi yake na si kwa kadiri ya matakwa au matendo yetu. Turuhusu nguvu ya Mungu itende kazi katika maisha yetu.
Injili: Katika somo la Injili tunasikia Kugeuka sura kwa Bwana wetu Yesu Kristu. Kugeuka sura kwa Yesu ni tukio muhimu sana kwa wanafunzi wake na kwa ulimwengu wote. Kwanza tukio hilo linaimarisha mioyo ya wanafunzi wa Yesu kuhusu Msalaba, (mateso ya sasa si kitu ukilinganisha na utukufu ule ujao, (Rum 8:18). Linawaimarisha imani yao juu mateso kifo na ufufuko wa Yesu. Na kwamba Yesu kachagua kwa hiari yake. Lakini pia linawafunulia Umungu wa Yesu, na pia Mungu anajifunua kuwa nasfi ya kwanza na kumtambulisha mwanae kuwa nafsi ya pili ya utatu Mtakatifu.
Kugeuka sura kunaonyesha ukamilifu wa fumbo la ukombozi wetu ndani ya Yesu. Yesu anakuwa katikati ya Musa, sheria, na Eliya, manabii na wanafunzi wake. Kristu ndiye utimilifu wa Agano la kale na agano jipya. Na ndio maana Mungu anamweka na kumtambulisha kama kiini/center ya ukombozi wetu. Anatuambia msikieni Yeye.
Mungu anatufunulia na kututoa woga na wasiwasi katika maisha yetu ya kihubiri Injili kwa matendo yetu ya toba, sala, kufunga na kufanya matendo ya huruma. Hiyo ndiyo safari yetu ya kumfikia Mungu, kuufikia utukufu wa Mungu kwa njia ya Mwanae Yesu Kristu.
Kwaresma ni kipindi cha kupanda mlimani. Kuwa karibu zaidi na Mungu. Hivyo lazima tuwe baraka kwa wengine. kupitia sisi wengine wabarikiwe. Dunia ione mwanga wa Injili. Tunapomtazama Yesu maisha anapogeuka sura na sisi maisha yetu yabadilike. Tabia zetu zibadilike, mawazo yetu yatakaswe, matendo yetu yabadilike, tutoke kwenye giza tuingie katika matendo ya mwanga.
Kupanda mlimani, kibiblia mara nyingi ni kuunganika na Mungu katika sala. Ndio moja ya nguzo zetu za kipindi hiki cha kwaresma. Kuunganika na Mungu. Ndio safari ya kushinda majaribu yale ya jangwani. Ndio mbinu ya kumshinda shetani. kuushinda uuovu, kushinda vishawishi. Tusikubali kubaki jangwani alipokuwa shetani anamjaribu Yesu, atatuchezea. Tupande mlimani kukutana na utukufu na utakatifu wa Mungu ili ung’arishe maisha yetu.
Tumwombe Mungu atujalie kuisikia na kuitii sauti ya Mwanae katika maisha yetu ili tuweze kushinda ulimwengu uliokubwa na dhoruba na majaribu ya jangwani. Tuombe utukufu wa Mungu ung’arishe maisha yetu na kutuondolea hofu na woga wa kulitangaza na kuliishi neno la Mungu.