Somo la Kwanza: YbS 15:15-20
Somo la Pili: 1 Kor 2:6-10
Injili: Mat 5:17-37
Somo la Kwanza: YbS 15:15-20
Somo la Pili: 1 Kor 2:6-10
Injili: Mat 5:17-37
Utangulizi
Mungu ametujalia akili na utashi. Akili inatusaidia kujua na utashi unatusaidia kuchagua mema na kuacha mabaya/uovu. Hivyo tunapochagua mema tumechagua uzima wa milele. Tunapochagua uovu/mabaya tunachagua moto na kuukataa uzima. Katika Dominika ya leo tuombe Roho atuongoze katika maisha yetu tuchague uzima wa milele kwa kuchagua na kutenda mema kwa kushika amri za Mungu.
Homilia
Mbele ya mwanadamu upo uzima na mauti. Naye amepewa uhuru wa kuchagua apendavyo. Ni Hiari yako ndugu mpendwa kuchagua moto au maji, uzima au mauti, Kuzishika amri zake ama kuzivunja. Tumepewa uwezo wa kutambua mema na mabaya, dhambi na kutenda mema, utakachochagua ndicho utakachovuna.
Somo la I: Katika somo la kwanza ndugu wapendwa, Yoshua Bin Sira anatuonyesha wazi kuwa Mungu ametupa uhuru wa kuamua ni nini cha kutenda, kusema, kufanya katika maisha yetu. Hivyo matunda yake yanatokana na utashi wetu wa kuchagua. Mungu amekuwekea mema, amri, neno lake, kwa ajili ya uzima wa milele. Utakapoacha kuchagua mema, uzima, amri na kuhukumiwa, baasi utakukumiwa kwa haki kwani umeacha mwenyewe kuchagua uzima.
Katika maisha yetu ya kila siku pia tumejaliwa uhuru huo wa kuchagua. Ukitaka kumchagua Bwana kwa kutenda haki, kuchagua mema unaahidiwa uzima wa milele. Umewekewa, sala, misa, majitoleo, zaka, amri, haki, wema n.k Ni hiari yako kuchagua. La, hutaki ni wewe unachajichagulia hukumu, na uwe tayari kuwajibika nayo.
Somo la II: Katika somo la pili, Mtume Paulo anatupa Mbinu ya kuchagua mema. Mbinu ya kutumia utashi wetu vizuri. Anasema ipo Hekima isiyo ya dunia hii. Wala watawala wa dunia hii hawaijui na hawakuijua.
Hekima hiyo imejificha katika Kristo, na inaletwa kwetu kwa Roho Mtakatifu. Hivyo tunapomwamini Kristo tunajaliwa kuchagua vyema. Na hivyo tukimtumaini na kumwamini Kristo, tunajaliwa uzima wa milele ambao umefichwa ndani ya Kristo Yesu nje na mafahamu yetu ya kibinadamu.
Injili: Katika somo la Injili ndugu zangu wapendwa, Kristu, ambaye siri ya ufalme wa mbinguni imefichwa ndani yake anafunulia namna ya kuziishi amri za Mungu, namna ya kuchagua mema, namna ya kuchagua uzima.
Kwanza yeye amekuka kutimiliza sheria. Amekuja kutia muhuri amri za Mungu. Pili anatuelekeza namna ya kuzishika na kuziishi amri. Haitoshi kuzijua na kuzitamka amri. Hata watu wengine wasio wakristu wanajua kujiepusha na mauaji, magomvi, uzinzi, uchawi, waganga, matambiko n.k.
Yesu anatutaka sisi tuende ndani zaidi ya huo mtazamo wa kawaida. Kwanza ianze ndani kabisa ya mioyo yetu. Midomo yetu isimwabu Bwana wakati mioyo yetu iko mbali na Bwana, rej. Mat 15:8, “watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami.” Hivyo haitoshi tu kuzijua amri na kuzitamka.
Yesu anatutaka tujue pia kuwa hatima ya kuzishika amri ni kwa ajili ya uzima wa milele. Huko ndiko kuchagua uzima wa milele. Hatusali ili tu tuhesabike kuwa wanaosali, hatuji kanisani ili tuonekane, hatuimbi ili kuonekana, hatuvai rozari ili tuonekane, hatufanyi ishara ya msalaba ili tujulikane waktisto wakatoliki, hatukemei udhalimu na uovu ili kupata umaarufu au kupata nafasi, bali ni kwa ajili ya uzima wa milele. Yote tufanyayo kama hayalengi uzima wa milele, basi tutabaki tu kama taasisi nyingine tu za kijamii.
Katika ufuasi wetu Yesu anatuasa kuutafuta uzima wa milele. Hatima ya yote tufanyayo kama wakristo ni kuokoa roho zetu na za wenzetu sisitupwe Jehanamu. Amri za Mungu ndizo kigezo na kielelezo cha kuwa tunachagua kutenda mema na kuacha uovu, kuacha dhambi.
Tumwombe Mungu atujalie hekima ya kimungu na tukisukumwa na upendo wa Kristo tujaliwe kutumia utashi wetu vizuri katika maisha yetu tusitumie uhuru wetu vibaya. Tuchague daima mema na kuacha uovu, tuchague haki na kuacha dhuluma, tuchague upendo tuache chuki, tuchague uzima tuache dhambi. Tumia uhuru wako vyema, chagua uzima wa milele.