Wewe ni Chumvi na Mwanga

2026-02-08
Dominika ya 5 ya Mwaka A
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Isa 58:7-10

Somo la Pili: 1 Kor 2:1-5

Injili: Matt 5:13-16

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Katika dominika ya leo Yesu anatukumbusha kuwa sisi ni chumvi na mwanga kwa wengine. Maisha yetu ya ufuasi yanatudai kuwa chachu ya upendo na msaada kwa wengine. Tunaalikwa kuukoleza ulimwengu kwa chachu upendo.

Homilia

Yesu anatukumbusha wito na wajibu wetu kama wakristo kwamba sisi ni chumvi na mwanga kwa ulimwengu. Tutakuwa chumvi endapo tutakuwa msaada kwa wengine na kuleta ladha ya maisha kwa wengine. Vivyo hivyo tutakuwa mwanga endapo tutawasaidia wengine kuona.

Somo la I: Katika somo la kwanza nabii Isaya anatupa njia chache za namna ya kuwa chumvi na mwanga kwa wengine. Matendo ya huruma kwa wengine. Kuwagawia wengine chakula, kuwasitiri wengine, kuwatembelea wenye shida, kuwagawia nguo wengine, kuwasaidai maskini, kuwahudumia wagonjwa n.k. Hii ndio namna ya kuwa chumvi na mwanga kwa wengine. Na tunapofanya hivyo Nabii anatuambia tunaita na Bwana ataitika.

Somo la II: Katika somo la pili Mtume Paulo anasisitiza kuwa hakuhubiri kwa hekima ya kibinasamu. Alihubiri kwa hekima na nguvu ya Roho Mtakatifu. Tunajifunza kuwa nguvu ya Injili si katika ufasaha wa maneno bali katika matendo ya maisha yetu. Paulo alitegemea nguvu ya Roho Mtakatifu. Alimtegemea Kristo.

     Nasi katika maisha yetu tusipomtegemea Roho Mtakatifu katika maisha yetu, hatutaweza kuwa chumvi, hatutaweza kuwa mwanga. Sehemu chumvi inatia ladha inapokuwa ndani ya chakula. Mwanga unatoa mwanga unapotoka kwa moto. Hivyo tunakuwa mwanga tunapounganisha Maisha yetu na Roho Mtakatifu. Tunakuwa chumvu tunapokuwa ndani ya Kristo.

Injili: Yesu anatumia mfano unaoeleweka katika mazingira ya maisha ya mwanadamu. Chumvi na Mwanga. Katika mazingira ya kawaida nay a kila siku tunatumia chumvi na tunatumia mwanga. Chumvi inakoleza ladha, chumvi inatunza, chumvi ni dawa. Mwanga unakuwa mwanga unapomwezesha mtu kuona. Yesu anatuambia sisi ni chumvi na mwanga.

     Tunaowajibu kwanza wa kujitambua kama chumvi na Mwanga. Tutakuwa tu mwanga tunapounganika na Roho Mtakatifu. Ili kitu kitoe mwanga kinahitaji kuunguzwa, burning. Hivyo tusipounganika na Roho mtakatifu katika maisha hatutaweza kuwa mwanga. Chumvi haiwezi kutia ladha isipoyeyuka. Inapoyeyuka inakoleza chakula, iponya kama ni kidonda, inatunza kamani nyama. Nasi tusipofungamanisha maisha yetu na Kristu, hatutaweza kukoleza ulimwengu kwa Injili, kwa upendo, kwa matendo ya huruma, kwa kutenda haki. Paulo amesema si umaarufu wa maneno yake, bali nguvu alliyochota katika Roho Mtakatifu na katika kufungamanisha maisha yake na Kristu.

     Na baada kujitambua kuwa sisi ni chumvi na mwanga, tunapaswa kuwa msaada kwa wengine. Katika matendo ya huruma. Kuwalisha wenye njaa, kuwahudumia wagonjwa, kuwaona wafungwa, kuwasaidia maskini. Kadhalika kuwafundisha na kuwaonya wanaopotea katika uovu, kuwaombea wenye shida, kuwasamehe wengine, kuwafundisha wengine, kuwaombea wafu.

     Hivyo ndugu wapendwa katika dominika ya leo Kristu anatuita tuwe chumvi na mwanga kwa ulimwengu. Kufungua dhamiri zetu, akili zetu na maisha yetu kwa matendo ya huruma ya kimwili na kiroho.