Achilia Nyavu Umfuate Yesu

2026-01-25
Dominika ya 3 ya Mwaka A
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Isa 8:23-9:3

Somo la Pili: 1 Cor 1:10-13, 17

Injili: Matt 4:12-23

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Leo ni Dominika ya 3 ya Mwaka A wa kanisa, Pia ni siku ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume. Yesu anatuita kuwa wafuasi wake, hivyo tunapaswa kuziacha nyavu, kutoka gizani na kumfuata yeye aliye Mwanga na Nuru ya Ulimwengu.

Homilia

Karibuni ndugu wapendwa katika Dominika ya Leo, Yesu anatuita kukoka katika giza na kuingia katika mwanga. Nchi ya Zabuloni na Naftali wanauona Mwanga Mkuu, Simon Petro na Adrea, na Yakobo na Yohane nduguye wanaziacha nyavu zao na baba yao wanamfuata Yesu. Anatutaka nasi kutoka katika giza la dhambi na kuachilia nyavu zetu na kuwa wakristu kweli.

Somo la I: Bwana anaturudishia matumaini na mwanga tena:

Katika somo la kwanza nabii Isaya anatoa unabii wa matumaini na ukombozi kwa nchi za Zabuloni na Naftali, wakati wa giza na kukandamizwa na kuvamiwa na Asyria. Walikuwa katika hali ya kukosa matumaini, kukata tamaa, na kukandamizwa. Na sasa wanapata ujumbe wa mwanga na matumaini kutoka kwa Bwana.

Tunajifunza kwamba daima Mungu yupo kwa ajili yetu. Wakati wa mateso, wakati wa kuonewa, wakati tukiwa gizani, wakati wa taabu, wakati tumedharauliwa, wakati tunalia; Mungu anatuletea furaha na Mwanga. Hii ni ahadi ya Bwana kwetu kwamba hajatuacha wakati wa shida na mateso, yupo kwa ajili yetu. Nabii Isaya ananena nawe leo, hali yako ya mateso itakuwa furaha, giza itakuwa mwanga, kilio itakuwa furaha, kudharauliwa kutakuwa kuinuliwa. Mtumaini tu na uliamini Neno Lake.

Somo la II: Yesu anatuunganisha kuwa kitu kimoja:

Matumaini na mwanga yasitoke kwa mtu, hata kama ni mzuri kiasi gani. Paulo anakataa. Kulitokea mgawanyiko huko Korinto wa wakristo waliojigawa wengine wa Paulo, wengine wa Apolo. Paulo anakuwa mkali. Anasema, Je Kristo amegawanyika?

Ni wazi kwamba hata katika maisha yetu kipo kishawishi cha kuweka matumaini yetu kwa watu maarufu, ama wahubiri maarufu. Tunakosea. Kristo ndiye tumaini letu, ndiye mwanga wetu. Paulo anatukumbusha kuwa tunayetakiwa kumtazama ni Kristo. Tukumbuke hata watu maarufu na wakubwa wanaweza kuanguka (2 Sam 12:1-12).

Injili: Somo la Injili limegawanyika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni utimilifu au ukamilifu wa Nabii Isaya tuliosikia katika somo la kwanza. Nchi ya Zabuloni na Naftali wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu. Yesu ndiye huo mwanga halisi unao ondoa giza la uovu. Ndiye matumaini yenyewe, ndiye wokovu halisi wa mwanadamu. Na mwaliko wake kwetu katika kutoga giza la dhambi na uovu ni “tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”

Sehemu ya pili ni kwamba Yesu anapoanza utume wake hadharani anaanza kwa kuwaita mitume wa kwanza. Anawaita na mara wanaziacha nyavu zao wanamfuata. Wengine wanamwacha baba yao, wanamfuata. Yesu anapowaita mitume hawa anatuita na sisi kwa majina yetu. Ndio maana ukristu ni ufuasi, ni kumfuata Yesu. Katika kumfuata Yesu ni lazima kuziacha nyavu zetu, ni lazima kutoka katika giza la dhambi.

Je! katika maisha yako, umekubali kuacha nyavu na kumfuata Yesu? Anakuita na kukuambia nifuate. Acha kung’angania madaraka, acha kung’ang’ania nymba ndogo, acha kung’ang’ania uzinzi, acha kung’ang’ania shughuli inayokunyima kusali dominika, acha kung’ang’ania kizuizi, acha kung’ang’ania giza, maisha ya kung’ang’ania matambiko. Maisha bila Yesu ni bure, Maisha bila ufuasi ni giza, maisha bila Yesu ni ubatili. Fanya maamuzi sasa. Penda maisha ya sala, maisha ya masakramenti, maisha ya kusimamia imani katoliki, maisha ya kuishi na kushika amri za Mungu.

Maisha ya imani yanatudai sadaka na kufanya mabadiliko. Hawa wanafunzi wanaziacha nyavu zao, wanamwacha baba yao, ni sadaka. Nawe achana na kinachokurudisha nyuma. Fanya mabadiliko kama ya Paulo. Paulo anapoongoka hageuki tena nyuma.

Yesu anatuita “Nifuata” tumwombe atujalie neema ya kuwa wafuasi wake kweli na kuwa wakristu kweli wa mwanga kwa wengine, kama walivyofanya mitume.