Somo la Kwanza: Isa 60:1-6
Somo la Pili: Efe 3:2-3, 5-6
Injili: Matt 2:1-12
Somo la Kwanza: Isa 60:1-6
Somo la Pili: Efe 3:2-3, 5-6
Injili: Matt 2:1-12
Utangulizi
Ukuu wa Yesu unafunuliwa Kwetu kupitia mamajusi kwa ishara ya nyota. Kristo ndiye Nyota halisi ya kutuongoza katika maisha yetu. Yeye anayejifunua kuwa nuru/mwanga wa mataifa yote, anatualika kuifuata nuru yake na kuishuhudia.
Homilia
Leo ni sherehe ya Yesu kujifunua na kujidhihirisha kwa mataifa yote. Mamajusi; Kaspari, Melkiori na Baltazar, kutoka mashariki wanawakilisha mataifa yote yanayoutafuta ukweli, Nuru ya wokovu.
Solo la I: Katika somo la kwanza, nabii Isaya anatabiri Yerusalemu kuangaziwa na utukufu wa Mungu. Na baada ya kuangaziwa nuru hiyo linatumwa kuwa nuru ya kuangaza na kuyaongoza mataifa mengine kwenye nuru hiyo.
Nuru hii si ya kibinadamu. Bali ni Mungu mwenyewe. Katika giza la dhuluma, chuki, uhasama, vita, kukata tamaa, - Kristo anakuwa taa na nuru ya matumaini na anatualika na sisi kuwa nuru na taa kwa ajili yaw engine kama Yerusalemu alivyokuwa nuru kwa mataifa mengine.
Somo la II: Solo la pili linadhihirisha kuwa Kristo ni mwanga na nuru kwa mataifa Yote. Hakuja kwa ajili ya watu fulan tu hapana, taifa moja tu hapana. Wokovu wa Kristo ni kwa wote bila ubaguzi. Hakuna tena mgeni mbele za Mungu.
Hii inatutaka kuvuka mipaka ya matabaka ya aina zote. Kuvuka mipaka ya ukabila, kijamii, kidini, kwa upendo kama ule wa Kristo. Sote tunavutwa kwake kwan ni Nuru na nyota ya kila mmoja.
Injili: Katika somo la Injili tunasikia mamajusi wanamtafuta mtoto Yesu na kuongozwa na nyota. Ili wakamwabudu na kumtolea zawadi. Lakini pia wanakutana ama kuitwa na Herode ambaye naye anamtafuta Yesu. Wote wanamtafuta Yesu bali nia zao ni tofauti.
Mamajusi wana nia ya kumtolea mtoto Yesu zawadi pamoja na kumwadudu. Hapa tunajifunza pia kuwa Yesu ndiye Nuru ya maisha yetu. Yesu ndiye dira ya maisha yetu, Yesu ndiye Mfalme wa Maisha Yetu, Yesu ndiye nyota ya maisha yetu, Yesu ndiye atupaye dira hasa kwa mwaka huu mpya. Ni namna gani atatuongoza, mamajusi wametuonyesha mfano. Mtafute anapatikana, yupo kwa ajili yako, Mwabudu katika sala, mtolee zawadi ya muda wako, zaka, majitoleo n.k. Msujudie yeye. Na kisha hapo maisha yako yatabadilika.
Herode naye anamtafuta Yesu. Lakini nia yake ni ovu. Anataka kumwangamiza. Kinachomsukuma ni nini? Hofu kwamba amezaliwa mfalme. Ubinafsi wa madaraka, kwamba hataki mwingine atawale. Ukaribu anaoutafuta Herode ni wa kinafiki. Urafiki anaoutafuta sio wa kweli. Wapo watu pia katika maisha wanaokutafuta ambao sio marafiki wa kweli. Wanakutafuta ili wakumeze, wakuangamize, wakuangushe, wakuabishe. Ndio maana vita kati ya ndugu na ndugu, familia na familia, majirani, n.k haviishi kwani kunakuwa na unafiki na woga kama wa Herode. Ndio maana wahenga wanasema, ili nyoka akuume lazima awe karibu na wewe. Basi angalia pengine wapo wanaokuchekea lakini kicheko chao haikitoki moyoni.
Tumwombe Yesu Mtawala awe mwanga na nuru katika maisha yetu na atujalie nasi tuweze kuwa nuru na mwanga kwa wengine tusiwe kama Herode na kusababisha giza ama kilio kwa mwengine bali tukishamsujudia tuweze kuiacha njia iendayo kwa uovu na giza na kutembea katika nuru yake.