Familia ni Neema

2025-12-28
Dominika ya Familia Takatifu
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Ybs 3:2-7

Somo la Pili: Kol 3:12-21

Injili: Mat 2:13-15, 19-23

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Katika sherehe za Noel tumesherekea Neema juu ya Neema. Yaani Yesu aliyezaliwa kwetu na kushiriki na ubinadamu wetu na kutushirikisha umungu wake. Leo tunaalikwa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya familia zetu.

Homilia

Familia iliyojengwa juu ya upendo, heshima na utiifu kwa Mungu huwa chanzo cha uzima na neema na matumaini kwa kanisa na jamii. Familia ni mfano hai wa maisha ya kikristo. Mfano wa familia bora ni familia ya Yesu, Maria na Yesefu.

Somo la I: Katika somo la kwanza, kitabu cha Yoshua Bin Sira inatupa na kutusisitiza umuhimu wa heshima kwa wazazi na baraka zinatokana na uhusiano mzuri na upendo katika familia.

     Heshima kwa wazazi inaleta baraka, maisha marefu na rehema za Mungu. Hivyo kila mmoja katika familia anatakiwa kutekeleza wajibu wake kiaminifu na kwa upendo. Mungu mwenyewe ameweka msingi wa upendo katika familia. Mtoto anayemuheshimu wazazi hujijengea hazina ya baraka na maisha marefu.

      Migogoro, kutokuwa na mawasiliano, kukosa adabu kwa wazazi, kutokuwajali watoto, kutokufunga ndoa takatifu, na kutowajibika ni baadhi ya mambo yanayoharibu familia za leo.

     SOMO LA II: Katika somo la pili Mtume Paulo anatupa maongozi ya maisha ya Kikristo ndani ya familia. Paulo anasisitiza fadhila za huruma, unyenyekevu, msamaha, subira, upendo kuwa ndio nguzo za maisha ya kifamilia.

     Upendo katika familia ndio gundi inayounganisha familia na kuifanya imara. Familia hazikosi changamoto, tofauti za mitazamo, makosa na majeraha. Lakini kinachotupa matumaini ni kwamba Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu licha kupitia changamoto lakini walibaki katika upendo daima. Kusameheana ndio nguzo pekee inayowezesha familia kuanza tena upya na kupyaisha maisha yao.

INJILI: Katika somo la Injili tunaona jinsi familia ya Yesu, Maria na Yosefu ilivyopitia hatari kubwa hata kukimbilia uhamishoni. Mahangaiko hayo ni makubwa.  Mahangaiko ya kutokuwa na hali ya usalama wa maisha na uhai. Jambo moja analohakikishiwa Yosefu ni usalama wa anakoambiwa na kuelekezwa na Mungu kupitia Malaika.

     Yapo mambo yanayohatarisha usalama wa maisha na uhai katika familia zetu. Katika familia za Kikristo mambo yanayohatarisha familia ni ukosefu wa sala ya pamoja, kukosa unyenyekevu, kukosa mawasiliano, ubinafsi, uchoyo, n.k

Mambo yanayoweza kuikoa familia katika hatari ya maisha, kama ilivyokuwa kwa familia ya Yesu, Maria na Yosefu ni kama yafuatayo:

     Familia Takatifu inatualika tuanze upya katika familia zetu. Tuwe na familia zinazomsikiliza Mungu, zinazolea dhamiri hai, zinazolinda uhai, na zinazoshuhudia upendo wa Kristo katika dunia ya leo. Familia zetu ni neema ya Mungu kwetu.