Somo la Kwanza: Hab 1:2-3; 2:2-4
Somo la Pili: 2 Tim 1:6-8, 13-14
Injili: Lk 17:5-10
Somo la Kwanza: Hab 1:2-3; 2:2-4
Somo la Pili: 2 Tim 1:6-8, 13-14
Injili: Lk 17:5-10
Utangulizi: Safari yetu ya maisha si rahisi. Mara nyingine tunapita kwenye wakati mgumu wa maisha. Tunapaswa kuwa na Imani. Nabii Habakuki anasema, jipe moyo mabaya yanapita. Paulo katika somo la pili anasema chochea Karama ya Roho Mtakatifu iliyo ndani yako na Injili Yesu anatuambia tuombe Imani. Tumwombe Mungu atuvushe katika yale magumu tunayoyapitia.
Somo la I: Kuna nyakati katika maisha tunakata tamaa kabisa. Tunakosa matumaini kabisa ya kuishi. Unajisikia kila mtu amekuacha. Na hata kuona kama Mungu naye amekuacha. Kuna nyakati ngumu sana katika maisha yetu. Lakini kinachotuokoa ni ukomavu katika imani yetu. Mungu anatuacha na anaruhusu nyakati hizo katika maisha ili tugundue: Maono ya Maisha yetu, Tupande maono hayo katika maisha yetu na tuishi katika maono hayo katika maisha yetu. Hii inawezekana kama tukistahimili hiyo mikiki mikiki katika maisha. Maana tumeambiwa Mwenye haki ataishi kwa imani yake.
Somo la II: Mungu alishapanda maono fulani kwako. Ameshapanda mbegu ya kitu fulani. Paulo anatuambia tuichochee karama hiyo. Mikiki mikiki ya maisha isitutoe kwenye reli na mstari wa maisha. Usikubali kuyumbishwa cha changamoto za maisha. Pambana, kuwa na imani, ondoa roho ya woga, Mungu hajatupa roho ya woga, bali ya nguvu na Upendo na ya moyo wa kiasi.
Injili: Fadhila ya imani ndio msingi wa mafanikio katika maisha yetu. Ndiyo inayotupa uvumilivu, ustahimilivu, upendo, matumaini n.k Imani itatuvusha katika dhoruba za maisha. Mitume wanatambua thamani ya imani na hivyo wanaomba kuongezewa Imani.
Katika masomo yetu tunajifunza kwamba:
Maisha hayakosi dhoruba: Kama tulivyosikia katika somo la kwanza, katika maisha kuna matatizo, magonjwa, kusemwa, kukataliwa, kuchekwa, kuchukiwa, kufiwa, kuumizwa, dhuluma n.k Ukimya wa Mungu usikupe shida. Jipe Moyo, kuwa na Imani Utashinda.
Imani haiwezi kudumu bila Roho Mtakatifu: Mt. Paulo katika somo la Pili anatueleza kuwa tunatakiwa kuichochea Karama ya Roho Mtakatifu tuliyempokea ndani mwetu ili tuweze kushinda mlima wa matatizo. Roho Mtakatifu anatupa nguvu ya kuvumilia, upendo na kiasi.
Thamani ya Imani: Yesu anatufundisha kuwa imani hata ndogo kiasi cha mbegu ya haradali, ina uwezo wa kuhamisha milima ya matatizo. Ina uwezo wa kugeuza maisha, kuponya majeraha na kukupa mafanikio katika maisha.
Imani ni Zawadi: Hakuna anayeweza kujisifu kuwa na Imani. Ukiwa na imani kweli unatambua kuwa ni Mungu ndiye aliyekupa zawadi hiyo. Ndio Maana mitume wanamuomba Yesu awaongezee Imani.
Imani inahitaji unyenyekevu: Mfano wa anatupa mfano wa mtumishi anayefanya wajibu wake bila kutafuta sifa. Kufanya mapenzi ya Mungu bila kujisifu, bila kujivuna. Imani ya kweli haihitaji kujisifu na kuonekana.
Ndugu zangu katika safari yetu ya matumaini tunahitaji Imani ya kweli. Safari yetu ina dhoruba na matatizo mengi. Bila imani tutakata tamaa. Bila imani tutakwama. Tusiogope, amini kwamba utashinda. Amini kwamba ipo siku Mungu atakuinua. Amini kwamba wakati wa Mungu ndio wakati sahihi. Tumwombe Mungu atuzidishie Imani.