Somo la Kwanza: Amo 6:1, 4-7
Somo la Pili: 1 Tim 6:11-16
Injili: Lk 16:19-31
Somo la Kwanza: Amo 6:1, 4-7
Somo la Pili: 1 Tim 6:11-16
Injili: Lk 16:19-31
Utangulizi: Maisha ya mwanadamu ya hapa duniani ni mara moja tu. Hakuna anayeishi mara mbili. Nafasi tuliyopewa ya kutenda mema ni mara moja tu. Na hiyo ndio kuepuka dhambi ya kutotimiza wajibu.
Somo la I: Katika somo la kwanza, Nabii Amosi anatoa onyo kwa matajiri wanaokula raha, bila kujali mahangaiko na mateso ya wenzao/wengine. Wanajisifia wao wanajisifia fahari zao na kusherekea kwa ubinafsi.
Mungu ndio anayetoa utajiri. Mungu ndiye tajiri wa kila kitu. Mungu anatupa utajiri kama mtihani wa namna ya kuishi na wenzetu. Mungu anapomnyima yule au anapowanyima wengine sio juu yetu. Bali sisi tunachopaswa kufanya ni kutenda mema daima kwa kadiri ya uwezo wetu.
Somo la II: Mtume Paulo anatupa mbinu za kukwepa kuhesabiwa hukumu ya kutokuwajibika kwa kutenda mema. Namna ya kuishi ya kumpendeza Mungu. Mambo hayo, mwalimu wa kwanza ni Kristo aliye mfano kamili wa maisha yetu. Nayo ni haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole. Mambo hayo yanatusaidia kukwepa dhambi ya kutokutiza wajibu na kutenda mema.
Injili: Katika somo la Injili tunapewa mfano wa wazi kuhusu tajiri na maskini Lazaro. Tunapewa picha ya maisha ya duniani na maisha ya mbinguni, maisha ya milele. Maisha yetu ya hapa duniani yana mchango katika maisha ya mbinguni. Kipimo tunachopewa ni kili kile cha Nabii Amosi; Tunapewa fursa, utajiri, mali, n.k ni namna gani tunakuwa wema katika kile ambacho Mungu ametujalia.
Katika masomo yetu tunajifunza mambo yafuatayo:
1. Kifo ni uhalisia wa Maisha. Katika kuishi kwetu lazima tujue kifo hakikwepeki. Hakuna utajiri unaoweza kuzuia kifo. Iwe tajiri, maskini wote tunakiendea kifo. Matumaini pekee ni kwamba Matendo yetu mema ndio yatakayotupa uzima wa milele. Tutahukumiwa kila mtu kwa nafsi yake namna alivyoishi hapa duniani. Daima tunaalikwa kusali, utuopoe katika kifo cha ghafla ee Bwana, ili tupate uzima wa milele.
2. Tunaishi mara moja tu hapa duniani: Maisha ya hapa duniani ni mara moja tu. Baada ya kufa hatuwezi kurekebisha tena chochote katika maisha tulioishi hapa duniani. Kama unataka kubadilika ndio sasa. Kama unahitaji kuandika historia nzuri ya maisha yako ni sasa. Tajiri aliomba apate mwanya wa kurudi hata kidogo lakini akaambiwa muda wako ulishapita basi.
3. Tunao Musa na Manabii: Katika kuishi kwetu Mungu anatupatia watu wa kutukumbusha kuishi maisha mema. Kutenda matendo mema. Moja ni kina Lazaro. Wahitaji katika mazingira yetu ni unabii na Injili kwetu tosha kuhushu kuishi maisha ya matendo mema. (Mt. 25: 30-46). Pili tanazo nyenzo mbalimbali: Neno la Mungu, Masakramenti, Watawa, Mashemasi, mapadre na maaskofu – wanaotukumbusha kutenda mema.
4. Kuepuka dhambi ya kukosa kufanya: Inawezekana kuzigawa dhambi katika makundi yafuatayo: dhambi za kiroho na kimwili au za mawazo, maneno, matendo na kukosa kufanya (sins of commission and omission). Katika Injili, tajiri hakumtukana Lazaro, hakumfukuza, sio yeye aliyemfanya maskini, hatuambiwi kama alipata mali kwa dhuluma. Kosa alilolifanya tu ni kushindwa kutenda wema kwa Lazaro. Nasi tunadaiwa kwa kushindwa kutenda mema, kushindwa kukemea uovu, kushindwa kufanya matendo ya huruma, kushindwa kuwasaidia wenzetu, kushindwa kutetea haki za wanyonge n.k tutadaiwa.
Hivyo ndugu zangu kutokujali ni dhambi. Mambo yanapoharibikia katika nyakati zetu na katika mazingira yetu nasi tusijali, tutadaiwa. Tumwombe Mungu atujalie tuweze kujiandaa na maisha ya mbinguni kwa kuepuka dhambi na kwa kutenda mema daima hasa kwa wahitaji.