Somo la Kwanza: Amo 8:4-7;
Somo la Pili: 1 Tim 2:1-8;
Injili: Lk 16:1-13
Somo la Kwanza: Amo 8:4-7;
Somo la Pili: 1 Tim 2:1-8;
Injili: Lk 16:1-13
Utangulizi: Mungu hachukii mali. Kwani vyote tulivyo navyo vimetoka kwake. Ameviumba Yeye. Anachotaka ni kwamba tunatakiwa tuvitumie kwa kumtukuza yeye na kudumisha upendo sisi kwa sisi. Tuombe neema ya kuwa na maarifa ya kuutafuta ufalme wa mbingu.
Somo la I: Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha nabii Amosi, tunapewa onyo kali kuhusu kuwagandamiza wengine kwa manufaa yetu wenyewe. Wakati wa Nabii Amos matajiri waliwanyonya maskini na fukara. Lakini tusiwanyoshee vidole. Hata sasa wapo. Katika nyakati zetu. watu wanatumia haki za wengine kujinufaisha wao binafsi. Wizi wa mali ya uma, kutokutenda haki, kurubuni haki za watu, kutumia kutokuelewa kwa watu kudhulumu haki zao n.k
Katika somo hili tunajifunza kuwa Mungu anachukia udhalimu anapenda na anataka kila mtu aishi kwa haki bila kudhulumiwa na bila kuonewa.
Somo la II: Mungu anadhihirisha alichomtuma nabii Amosi katika somo la pili. Mungu anataka kila mtu apate wokovu. Wokovu ni kwa wote. Wokovu huo tumeupata Kupitia Yesu Kristo; mpatanishi kati ya Mungu na Mwanadamu. Si mpatanishi kati ya Mungu na matajiri, hapana, Mungu na wafalme, hapana, Mungu na wakuu, hapana. Ni Mungu na sisi sote. Ndio maana anataka tuwaombee hata wafalme, wakuu, viongozi ili kusudi wapate wokovu pia wasipotee kwa udhalimu.
Injili: Yesu anatumia mfano wa tajiri mwerevu aliyeweza kujiokoa katika kupata aibu. Sio kwamba Yesu anahalalisha ujanja la hasha. au dhuluma la hasha. Bali anatutaka vile tunavyoweza kujanjaruka na Mali za duniani kadhalika na kuchangamkia Fursa za uzima wa milele. Ndio maana mwishowe anasema hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Ndio maana Yesu anatutaka kujifunza mambo yafuatayo;
Uaminifu katika mambo madogo: Ni ukweli usiopingika kwamba, uaminifu unaanza kupotea katika mambo madogo kabisa. Mwizi haanzi katika kuiba milioni. Alianzia na shilingi moja, na polepole anajikuta jambazi. Mpigaji wa mamilioni alianza na makando kando madogo.
Mali za Dunia hii ni ya Kupita; Daima tusijisahau na utajiri na mali za hapa duniani. Ni za muda na za kupita. Dunia ni maptito wenyeji wetu ni wa mbinguni. Huko ndiko pa kuchangamkia zaidi. Mali za dunia zinatolewa kama mtihani kupima uaminifu wetu kwa Mungu na upendo kwa jirani zetu.
Hatuwezi kumtumikia Mungu na mali: Ni ngumu kuelewa ni kama vile Mungu hatakaki tushike mali au tushike fedha. Lakini sivyo. Fundisho hili ni kwamba tusifanya mali au utajiri ndio umungu wetu. Kwamba tukishakuwa na mali tuziabudi kiasi cha kumsahau Mungu na kutokuwa na hofu ya Mungu tena. Nabii Amosi anatuonya na Yesu pia anatukataza.
Hivyo Tumwombe Mungu atujalie kuweza kutumia mali zetu na utajiri wetu kwa kumtukuza Yeye aliyetupatia na kuzidisha upendo kwa jirani na hasa maskini na wasiojiweza.