Somo la Kwanza, Hes 21:4b-9;
Somo la Pili: Flp 2:6-11;
Injili: Yn 3:13-17
Somo la Kwanza, Hes 21:4b-9;
Somo la Pili: Flp 2:6-11;
Injili: Yn 3:13-17
Utangulizi: Msalaba ni ishara kuu ya wokovu wetu, upendo, matumaini, uponyaji. Katika sherehe hii ya kutukuka kwa Msalaba ni kwa ajili ya kutukumbusha kuwa Msalaba dawa yetu ya kutuponya. Tunaalikwa tujivunie Msalaba wa Yesu na tuutazame kwa imani.
Somo la I: Katika somo la kwanza tunaalikwa ndugu zangu kutazama nyuma kwa shukrani. Kutazama mema ambayo Mungu katujalia bila hata mastahili yetu. Waisraeli Walimnung’unikia Mungu walipokuwa jangwani, wakaadhibiwa kwa nyoka wa sumu. Musa akapewa amri amtengeneze nyoka wa shaba, na yeyote atakayemtazama ataokoka.
Ndugu zangu baada ya kunung’unika dhidi ya Musa na Mungu, wana wa Israeli walipewa adhabu ya kugongwa na Nyoka kufa. Kwa sababu walimsahau Mungu aliyewatoa utumwani. Mungu anaokoa tena kwa ishara hiyo ya nyoka wa shaba.
Nasi Mungu ametuwekea ishara hiyo ya msalaba tunapomsahau. Tunaposhindwa kumshukuru Mungu kwa yale aliyotutendea. Tunaposhindwa kuona yale Mungu aliyotuvusha katika maisha.
Somo la II: Katika somo hili tunaona Msalaba unatufundisha unyenyekevu, sadaka, majitolea, kujishusha. Paulo anatufundisha kwamba Kristo ingawa ni Mungu, alijinyenyekeza akawa mtumishi, akajitoa hadi kifo cha msalaba.
Msalaba huo ndio tunaojivunia wokovu uliotundikwa juu yake. Msalaba wa Kristo unatupa nguvu ya kupokea magumu katika maisha na kuyaendea kwa imani.
Injili: Katika somo la Injili tunapata utimilifu wa ishara ile ya nyoka wa shaba aliyeinuliwa juu. Yesu anatuonyesha kuwa, ishara ile ni Yeye aliyeinuliwa juu ya msalaba ili sisi tupone. Na ni kweli sisi tumepona kwa sababu ya Msalaba.
Msalaba umetufungulia njia ya Mbinguni. Kwa kuinuliwa kwake msalabani na kufa na kufufuka sisi tumepata mtangulizi na njia ya kufika mbinguni.
Tumwembe Mungu atuongezee imani ili tuweze kuponywa na msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo.