Somo la Kwanza: YbS 3:17 – 20, 28 -29
Somo La Pili: Ebr. 12:18 – 19, 22 – 24
Injili: Luka 14:1, 7 – 14
Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe nay eye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele Zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
Utangulizi: Ndugu zangu wapendwa leo tunaalikwa kuishi fadhila ya unyenyekevu katika maisha yetu. Fadhila hii inatuwezesha kushinda majivuno, ukaidi, kiburi, udhalimu, kujikweza, kujisifu, ubinafsi, na zaidi ya hayo kwa fadhila ya unyenyekevu ndipo Mungu anatuinua (Flp 2:2-6)
Somo la I: Katika somo la kwanza tunasikia wosia wa mzazi kwa mwanae. Kwamba kadiri Mungu alivyomjalia Baraka zake ni kadiri hiyo hiyo anapaswa kuwa myenyekevu. Kadiri Mungu anavyokujalia kujua mengi na kujifunza mengi ndivyo unavyopaswa kuwa mnyenyekevu. Katika ulimwengu wa mwandishi inaonekana kulikuwa na intellectual pride, hasa ya elimu falsafa ya kihellenistic, (Helenistic Philosophy). Pengine elimu hii dunia iliwafanya waone hata elimu ya Mungu, na kumkiri Mungu hakuna maana. Ndio maana baba huyu anamuasa mwanae awe mnyenyekevu.
Hata sisi tunakuwa na majivuno na kiburi pale tunapojaliwa kujua, kujaliwa maisha fulani, bahati fulani, tunajiona kuwa ni miungu na hatumuhitaji Mungu. Ndio maana tunawatesa wengine kwa sababu ya elimu yetu, kujua kwetu, kujaliwa kwetu, kubarikiwa kwetu n.k. Yoshua Bin Sira anatuambia leo, Kadiri tunavyojaliwa, elimu, uwezo, nguvu, maisha n.k ni kadiri hiyo hiyo tunatakiwa kuwa na unyenyekevu. Tunapaswa kujua kwamba kwa Bwana ndipo hutoka maarifa na ufahamu wa kweli (Hek 2:6). Wale wanaojaliwa ufahamu na hasa wa hekima ya Mungu hawasemi sana, na wanapendwa kuliko yule anaefahamu kidogo na anapiga kelele mtaa/mji mzima.
Somo la II: Katika somo la pili tunakumbushwa namna Mungu alivyofanya agano nasi. Kwanza alifanya agano Mlimani Sinai. Agano lililofanyika hapa duniani. Pili amefanya agano nasi Mbinguni, agano jipya. Agano hili alifanya na Mwanae, na sio tena kama Waisraeli walivyoogopa kugusa mlima ukiwa unafoka moto (Kut 19), bali kwa damu ya Mwanae, Bwana Wetu Yesu Kristo, tunaweza kumfikia Mungu. Mungu ameturuhusu tumfikie kwa unyenyekevu wa Mwanae (Flp 2:2-6), na ili kumfikia lazima tuwe wanyenyekevu.
Injili: Mwinjili Luka anatuambia, ufalme wa Mungu unapatikana kwa kuwa mnyenyekevu. Kujushusha mbele za Mungu. Kuingia katika ufalme wa Mungu, Katika karamu ya Mungu, sio kwa nafasi yako, kwa umaarufu wako, kwa ukubwa wako, bali ni katika kukubalika na Kristo mwenyewe, atakayekukaribisha. Kwa mazingira ya kiyahudi walijiona kwamba wapo wanaostahili na wasiostahili. Ndio maana anamalizia na kuwa marafiki na maskini, vilema, vipofu, viwete, kwa kuwa hawana cha kukulipa. Yesu anatuambia, anayetustahilisha mahali pa kuketi harusini ni yeye, Bwana Harusi mwenyewe.
Ndugu zangu wapendwa katika somo la Injili na somo la kwanza tunasisitizwa kuwa wanyenyekevu katika maisha yetu. Mambo machache yanayoonyesha ukosefu wa unyenyekevu katika maisha yetu:
Kujihesabia haki: Pale ambapo katika maisha yetu tunapojihesabia haki kwamba mimi nastahili kuwa hapa. Yesu anasema subiri uonyeshwe pa kuketi.
Kujifanya wajuaji: Pale ambapo tunataka kutoa majibu ya kila swali na kila jambo. Hatukubali ushauri na mtazamo wa mwingine. Yoshua Bin Sira anasema, mwanangu kwa machache uliojaliwa kujua, kuwa mnyenyekevu.
Kujiweka tabaka la juu: pale ambapo unaona wengine hawastahili. Namna ambavyo walivyochagua viti vya mbele. Kwamba vya nyuma kuna wenyewe. Kristo anatutaka kuwa wanyenyekevu.
Kutokusali: Ishara ya kutokujiweka chini ya maongozi na ulinzi wa Mungu. Tunajiona kuwa kuishi ni haki yetu, maisha na uhai ni haki yetu na sio zawadi ya upendo wa Mungu kwetu.
Kutokukiri Makosa yetu: Hii ni ishara ya kiburi mbele ya Mungu na wanadamu wenzetu. Tunang’ang’ania kwamza tuko safi, hatuna dhambi. tuko sawa hatujateleza.
Unyenyekevu hushinda ukarimu, unyenyekevu unatustahi tusiaibike, unyenyekevu ni ishara ya kutambuwa uwepo wa Mungu katika maisha yetu, unyenyekevu ni ishara ya kujifunza zaidi. Tumwombe Mungu atujalie fadhila hii Muhimu katika maisha yetu, tukijifunza kwa Kristo mwenyewe aliyejinyenyekeza hata Mauti ya Msalaba.