Sadaka Bila Imani Ni Mchango

2025-08-10
Dominika Ya 19 Ya Mwaka, C
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

 

Somo la Kwanza Hek 18:6-9

Somo la Pili Ebr 11:1-2, 8-19

Somo la Injili

Lk 12:32-48

Yesu aliwaambia makutano: Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme. Viuzeni mlivyo navvo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa. akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu. Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; nanyi iweni kama watu wanaomng jea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara. Heri watumwa wale, ambao bwana wao ajapo atawakuta wanakesha. Amin, nawaambieni, atajifunga na kuwa- karibisha chakulani, atakuja na kuwahudumia. Na akija zamu ya pili, au akija zamu ya tatu, na kuwa kuta hivi, heri watumwa hao. Lakini fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu. Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu, au watu wote pia? Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, arnbaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, arnbaye bwana wake ajapo atamkuta anafanva hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini, mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. Na mtumwa yule aliye  jua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, nave amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi:

Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, bayana ya mambo yasiyoonekana. Imani ni kuwa na hakika na kutarajia kwamba matokeo ya maisha tunayoishi sasa ni katika ulimwengu ujao, katika ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo. Na ndio maana tunapotoa sadaka kwa imani, tunaamini tunamtolea Mungu.

HOMILIA

Somo la I: Katika somo la kwanza, kitabu cha Hekima ya Sulemani kinasimulia usiku ule ambao baba zetu walikesha wakati wa pigo la kumi la Wamisri, walipouwawa wazaliwa wa kwanza wa Wamisri. Kwa imani wazee hawa walikesha na kuutazamia wokovu wao kutoka utumwani Misri. Na walimtolea Mungu dhabihu kwa siri.

     Ndugu zangu wapendwa tunajifunza kwao kwanza Imani kubwa kwa Mungu, kukesha na kuutazamia Wokovu wa Mungu. Hakuna sala inaenda na sadaka. Walimtolea Mungu dhabihu kwa siri. Hivyo wanatuonyesha namna sala inavyoenda na sadaka; ya muda, ya majitoleo, kujitoa, na imani kubwa ya ukombozi ujao.

Somo la II: Katika somo la pili tunapata ufafanuzi mzuri wa imani na sadaka. Ibrahimu na Waisraeli ni mifano kwetu wa Imani walioionyesha ya kutarajia ukombozi kutoka utumwani, na kutazamia nchi ya ahadi. Bila kujali na kujua wanakoenda kukoje, walikesha na kushika njia.

     Ndugu zangu ulimwengu wetu wa sasa unadanganyika na imani ya ushuhuda kwanza badala ya kujikabidhi kwanza kwa Mungu. Watu wanataka waone kwanza yakitokea ndipo waamini. kumbe, Imani ni kuwa na hakika ya Mambo yatarajiwayo, yasioonekana. Wazee wetu wanashuhudia hiyo. Kuitazamia nchi ya ahadi kwa imani kubwa. Nasi tuitazame Mbingu kwa imani kubwa.

     Pia tunaona Imani inabadili lisilowezekana kuwezekana. Kwa Imani Sara anapata mimba, licha ya kwamba alikuwa mzee. Kwa imani hakuna lisilowezekana kwa Mungu.

     Tunaona tena imani kubwa ya sadaka ya Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoe mwanae Isaka awe dhabihu. Sadaka iliyounganika na imani kubwa. Imani hiyo Mungu anatupa picha ya Kristo Yesu ambaye Mungu alimtoa mwanae wa pekee kwa ajili ya uzima wetu.

Injili: Katika somo la Injili Kristo anatuzamisha zaidi katika kuutazamia na kuutarajia uzima wa milele. Kwanza, anatutoa mashaka sisi kundi dogo, {pengine unapojiona kutengwa, kudharauliwa, kukataliwa, kubaguliwa, n.k} kwamba yeye ametuletea ukombozi na tunaahidiwa ufalme tukisimama imara katika imani.

     Pili anatuzamisha tumtolee Mungu dhabihu ya shukrani kwa ajili ya ufalme wa Mbinguni. Tuwekeze Mioyo yetu kwenye ufalme wa Mbinguni. Tujiwekee hazina mbinguni, ambapo hakuna kutu wala mwizi. Hii lazima itolewe kwa imani kama ilivyokuwa sadaka ya Ibrahimu. Mara nyingi tunapotoa sadaka zetu hatutofautishi na michango mingine kama vile kwenye harusi, vikoba, n.k.

     Katika sehemu ya tatu ya Injili, Yesu anatutaka tutoapo sadaka basi tuiunganishe na utazamio wa ujio wa pili. Kwamba kama waisraeli walivyotolea dhabihu kwa siri kwa ajili ya kuutazamia ukombozi kutoka utumwani, na Ibrahimu alivyomtoa mwanae Isaka kwa ajili ya Imani yake kwa Mungu, Nasi majitoleo yetu, sadaka zetu zisipounganishwa na kuutazamia ujio wa ufalme wa Mungu, na hasa kututoa katika utumwa wa dhambi basi itakuwa si dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu. Kwani hata utoe mchango mkubwa kiasi gani, na bado unang’ang’ania dhambi, haisaidii.

    Hivyo ndugu zangu wapendwa, leo tunakumbushwa kwamba, tuwe na imani kubwa hasa ya kuutazamia ufalme wa Mungu. Sala zetu zinatudai sadaka, na sadaka zetu zinatudai imani, kutoa kwa imani. Na Sadaka zetu zinatakiwa zituzamishe katika kuutazamia ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo.