Somo la Kwanza: Kumb 30:10–14
Somo la Pili: Kol 1:15–20
Somo la Injili: Lk 10:25–37
Siku ile, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu, akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyanyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.
Somo la I
Musa anawaandaa wana wa Israeli kwenda kuishi katika nchi ya ahadi. Anawaambia Neno la Mungu, maagizo yake na Sheria yake vipo katika mioyo yao. Sheria ya Mungu haipo mbali nao ipo kwa vinywa vyao na mioyo yao. Hivyo hawana sababu ama kisingizio cha kutokutii Neno la Mungu, amri za Mungu, maagizo ya Mungu.
Neno la Mungu, sheria za Mungu, maagizo ya Mungu, yapo katika mioyo yetu yapo katika dhamiri zetu. Tunapo vunja amri za Mungu si kwa bahati mbaya tunakiuka na kuziba masikio ya dhamiri zetu hai zilizo ndani yetu. Mungu anatukumbusha daima kulisikia Neno Lake na kushika Amri zake kwa dhamiri zetu.
Somo la II
Katika Kristo vitu vyote viliumbwa. Katika yeye sisi tuliumbwa. Yeye ndiye Neno la Mungu aliyefanyika mwili akakaa kwetu. Kupitia yeye tunapatanishwa na Mungu.
Tunapomkiri Kristo, dhamiri zetu zinakuwa hai. Tunaisikia sauti yake, tunatii amri zake, tunatii neno lake. Yeye anatukumbusha daima katika mioyo yetu kuhusu amri zake, neno lake na maagizo yake.
Injili
Yesu anatupa mfano wa Msamaria mwema anayeitii dhamiri yake njema. Yesu anamjibu mwanasheria anayemjaribu. Ukweli ni kwamba tusiposikiliza dhamiri zetu njema, tusipomsikiliza Mungu anayesema nasi kwa amri zake na maagizo yake katika mioyo yetu tunakosa kuwa watu wa upendo na huruma kwa wenzetu.
Mazingira yetu yamejaa ulawi, kila mtu apambane na hali yake, hata kama anakaribia kufa. Tunakosa upendo na huruma. Tunakosa kuwa ujirani mwema. Tunaishi ulawi badala ya usamaria, badala ya ujiran mwema.
Yesu anatukumbusha kwamba vyeo vyetu, hadhi yetu, kabila letu, kazi yetu, utamaduni wetu n.k visitutenge na upendo na huruma ya Mungu kwa wengine. Vitusaidie kuamsha dhamiri zetu juu ya ubinadamu wetu na upendo kwa jirani.