Utatu Mtakatifu, Ufunuo wa Asili ya Mungu Kwetu

2025-06-15
Dominika ya Utatu Mtakatifu
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza, Mit 8: 22-31

Somo la Pili, Rum 5:1-5

 Injili, Yn 16:12-15 

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Utatu Mtakatifu ni Mungu Mmoja katika nafsi tatu. Upendo wa Mungu kwetu unajidhihirisha katika nafsi tatu. Ingawa tunaweza kuona kazi ya Baba, Mwana, au Roho Mtakatifu kwa uwazi zaidi katika hali fulani, lakini hata hivyo hatuwezi kuachanisha nafsi moja na nyingine. Muunganiko huo wa upendo ni mwaliko kwetu kuishi kwa upendo na muuunganiko na jirani.

Homilia

Kila tunapoaanza na kumaliza sala zetu tunatumia fumbo la Utatu Mtakatifu. Ishara ya msalaba. Kadhalika wakati wa ubatizo (Mt 28:19). Fumbo la utatu Mtakatifu linafundisha yafuatayo: Baba ni Mungu, Mwana ni Mungu, na Roho Mtakatifu ni Mungu. Hata hivyo hakuna miungu watatu bali Mungu mmoja katika nafsi tatu. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ndio asili ya Mungu aliyopenda kujifunua kwetu na kuwa nasi kwa karibu zaidi. Katika Biblia hatuna neno utatu lilikotajwa kwa wazi. Lakini tunashuhudia uwepo wa kazi ya uumbaji wa dunia kwa Mungu Baba (Mwa 1:26). Lakini Mungu anatumia wingi. Hii inadhihirisha uwepo wa Divine council, uwepo wa baraza la Mungu, ambapo baadhi ya wataalamu husema hapo ndipo nafsi tatu zipoanza kujifunua kwetu. Hii inadhihirishwa katika somo la kwanza katika kitabu cha Mithali, tunaona Hekima ama busara katika uumbaji.

Mungu anamtumia Hekima katika uumbaji. Paulo anatuambia wazi wazi kwamba katika Kristo vitu vyote viliumbwa (Kol 1:16). Hivyo kwa uchache tunaona nafsi ya Baba na Mwana zikidhihirishwa katika uumbaji katika umoja na kila moja ikijidhihirisha katika kazi yake. Katika somo la pili, Paulo anakazia kwama kupitia Kristo tunafikia neema ya kufurahia utukufu wa Mungu. Na Pendo la Mungu linamiminwa kwetu na Roho Mtakatifu. Nafsi ya tatu inadhihirishwa wazi. Injili inatudhihirishia kuwa tunamfikia Mungu kupitia Utatu Mtakatifu. Yesu anazungumzia kuja kwake Roho wa Kweli. Na huyo Roho wa Kweli hatanena kwa shauri lake mwenyewe. Atayanena atatwaa katika yaliyo ya Kristo, na hayo ya Kristo ni ya Baba. Hapa ndipo tunapofunuliwa kuwa Mungu ni Mmoja katika nafsi tatu. ni katika kutupenda na kutufikia sisi anajifunua kwetu katika nafsi tatu.

Fumbo hili linapita upeo wa kibinadamu. Lakini haizuii kuliona ama kung’amua ukweli uliopo katika fumbo hilo kwa macho ya Imani. Paulo anasema, kama mtu unajifahamu kupitia nafsi yako mwenyewe na sio nafsi ya mwingine basi vivyo hivyo Mungu anajulikana tu katika Roho wa Mungu (Rum 8:14-17) Kumbe Fumbo hili – sio kwamba linamfanya Mungu awe mbali nasi, la hasha. bali Mungu anakuwa karibu zaidi na sisi, katika maisha yetu, katika kazi zetu, katika masomo yetu, biashara zetu, katika utawa wetu katika ukristo wetu : ndio maana tunautukuza utatu katika kila tunaposali: Ishara ya msalaba, sala ya atukuzwe, sala ya zetu tunazipeleka kwa Mungu kupitia Roho Mtakatifu. Na zaidi ya yote tunaadhimisha ekaristi takatifu katika utatu mtakatifu. Hili fumbo likakuwa gumu kwetu kwa sababu tunajitenga na Upendo wa Mungu – ambao yeye mwenyewe anajifunua kwetu.

Tunapokuwa katika hali ya dhambi, katika chuki, katika mafarakano, kutokuelewana, kutokusikilizana, kutokusaidiana, kutokujaliana, kutokusaidiana n.k mambo hayo yanapingana na umoja tunaouadhimisha katika Utatu Mtakatifu. Kumbe tunapoishi katika upendo, katika kushika amri tunatambua fumbo hili katika maisha yetu. Hatutasali tena sala zetu kwa mazoea tutazisali kwa kuuishi utatu Mtakatifu tunaopata neema zake katika ubatizo.